Friday, 26 May 2017
MIAKA 4 YA TASAF NA MAFANIKIO CHANYA KATIKA MIRADI YAKE
Wadau wa maendeleo wanaochangia fedha za utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF nchini wameonyesha kuridhishwa na kasi ya kupambana na umaskini kupitia mpango huo ulioanza kutekelezwa takribani miaka minne iliyopita.
Wadau hao wa maendeleo kutoka nchi na mashirika kadhaa ya misaada ya kimataifa wameonyesha kuridhishwa na namna walengwa wa Mpango huo wa kunusuru kaya maskini wanavyotumia fedha za ruzuku katika kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi inayowaongezea kipato na kuwawezesha kuboresha maisha hususani katika sekta za elimu,afya na kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba za kudumu.
Wadau hao ambao wako kisiwani Zanzibar wameweza kuona namna walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini wanavyonufaika na shughuli za Mpango huo,wametembelea shahia ya Potoa kaskazini Unguja ambako wamekutana na walengwa wa Mpango huo na kujionea shughuli walizozianzisha kwa kutumia fedha ya ruzuku inayotolewa na serikali kupitia mpango huo.
Aidha Mwakilishi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia, Bwana Muderis Mohamed amesema kasi ya walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini nchini Tanzania ni ya kuvutia na kutia matumaini makubwa ya kupunguza umaskini miongoni mwa walengwa kutokana na mwitiko mzuri wanaouonyesha katika matumizi ya fedha na uanzishaji wa miradi midogo midogo ya kiuchumi kwa kutumia fedha za ruzuku zinazotolewa na serikali kupitia TASAF.