WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Bibi Tecla Hamidu ambaye
ni mlemavu wa miguu sh. milioni tano ili aweze kuongezea katika mtaji wake.
Ametoa fedha hizo leo (Jumanne, Machi 20, 2018) ikiwa ni katika
kutimiza ahadi yake aliyoitoa Februari 22, 2018 kwenye Mkutano wa Sita wa
Wamiliki wa Viwanda na Watumiaji wa simbomilia (barcodes).
Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo baada ya Bibi Tecla ambaye ni
mjasiriamali anayejihusisha na ushonaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo
kumuomba amchangie sh. 500,000 ili aweze kuongezea mtaji wake.
Wakati akimkabidhi fedha hizo, Waziri Mkuu amesema kwamba
anatarajia zitamsaidia katika kuongeza mtaji wake, hivyo atazalisha
bidhaa nyingi zenye ubora unaohitajika katika masoko ya ndani na nje.
Kwa upande wake, Bibi Tecla alimshukuru Waziri Mkuu kwa msaada
huo na ameahidi kuzitumia fedha hizo kama ilivyo kusudiwa.
“Nashukuru kwa msaada huu kwani kuna watu wanakopa sh. laki
mbili ili waongeze mitaji, lakini mimi leo nimepewa milioni tano bure na
kiongozi wetu,”
Amesema licha ya kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa
masoko anaamini tatizo hilo litakuwa historia baada ya kuwa na mtaji wa kutosha
kwani atakwenda kuzalisha bidhaa zenye ubora zaidi.